top of page

Kijue Chama cha Mapinduzi na Historia yake

>Ilani ya Uchaguzi 2020-2025

CHAMA CHA MAPINDUZI

 

 

HISTORIA YA CCM TANGU TANU NA ASP

 

 

Imetolewa na Idara ya Itikadi na Uenezi kwa ajili ya Semina za Halmashauri Kuu za Taifa, Mikoa na Wilaya. Inapatikana pia katika kitabu cha Sera za Msingi za CCM

 

Makao Makuu ya CCM

 

Dodoma, 2004

 

HISTORIA YA CCM TANGU TANU NA ASP

 

1.0 UTANGULIZI:

 

Maelezo ya awali

 

Chama cha Mapinduzi (CCM) kilizaliwa tarehe 5 Februari, 1977 kutokana na kuvunjwa kwa vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP).

 

Tendo hilo la kihistoria lilikuwa ni la kuendeleza utamaduni uliokuwa umeanza huko nyuma wa kuunganisha nguvu kwa lengo la kujiimarisha katika mapambano. Kwa mfano, ASP kwa upande wa Zanzibar ilitokana na kuungana kwa African Association (AA) na Shirazi Association (SA), tendo ambalo liliunganisha nguvu za wanyonge katika mapambano ya kuundoa usultani na utawala wa kikoloni wa Kiingereza. Kwa upande wa Tanzania Bara, TANU ilitokana na kujibadilisha kwa Tanganyika African Association (TAA) kutoka jumuiya ya kutetea maslahi ya kijamii na kuwa chama cha siasa.

 

Kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika tarehe 9 Desemba, 1961 na ule wa Zanzibar kupitia Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964, kulifanya TANU na ASP viwe vimekamilisha jukumu la ukombozi wa nchi hizi kutoka makucha ya ukoloni mkongwe na usultani. Hata hivyo, vyama vya siasa hivi viliendelea kukabiliwa na majukumu ya kuendeleza mapambano ya ukombozi katika Afrika na kote duniani; kujenga Tanganyika na Zanzibar huru kiuchumi na kijamii na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa,

 

Katika mazingira ya ubeberu duniani wakati huo na hali ya unyonge wa mataifa haya machanga, yakielewa kuwa ‘umoja ni nguvu’, Tanganyika na Zanzibar zilibaini umuhimu wa muungano, hivyo ziliamua kuungana tarehe 26 Aprili, 1964. Muungano huo ndio uliowezesha kuzaliwa kwa Tanzania. Chini ya Muungano huo, Tanzania iliendelea kuwa na vyama vya siasa viwili, yaani TANU na ASP katika mazingira ya chama kimoja cha siasa. Vyama hivi vilitambua fika kwamba vinahitaji chombo madhubuti cha uongozi katika kutekeleza majukumu yake ya ukombozi kwa ukamilifu hivyo uamuzi ulifanywa rasmi wa kuvunja TANU na ASP na kuundwa kwa Chama Cha Mapinduzi tarehe 5 Februari, 1977.

 

Katiba ya CCM, katika Azimio la Mkutano Mkuu wa Taifa wa Pamoja wa TANU na ASP tarehe 21 January, 1977, inaeleza kuwa, (uk. 2-3), “...kwa kauli moja tunaamua na kutamka rasmi kuvunjwa kwa Tanganyika African Union(TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP) ifikapo tarehe 5 Februari, 1977 na wakati huohuo kuundwa kwa Chama kipya cha pekee na chenye uwezo wa mwisho katika mambo yote kwa mujibu wa Katiba.”

 

Muungano wa TANU na ASP ndio uliowezesha CCM kuwa Chama chenye nguvu, imara na madhubuti, hivyo kuwa Chama cha siasa pekee chenye uwezo wa hali ya juu wa kuwaunganisha Watanzania. Aidha, CCM kimeweza kuwaongoza wananchi katika mapambano ya kitaifa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kufuatana na mabadiliko mbalimbali yanayojitokeza ndani na nje ya nchi.CCM kimeendelea kupewa dhamana na wananchi ya kuunda serikali na kukamata dola tangu 1977 chini ya mfumo wa demokrasia ya chama kimoja hadi sasa katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, kufuatia mageuzi yaliyoidhinishwa na marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Tanzania Juni 1992.

 

1.2 Umuhimu wa kuielewa historia ya CCM na Vyama vilivyokitangulia

 

Historia ya CCM tangu TANU na ASP ina umuhimu wa pekee katika Taifa letu katika kuelewa tulikotoka, tulipo hivi sasa na tunakoelekea. Historia ya nchi yetu haiwezi kukamilika bila ya historia ya vyama hivi vya ukombozi. Historia hutoa mafunzo na ni mwelekezaji pia, kwa hiyo ni wajibu wa Watanzania, hasa wanachama wa CCM kujifunza kutokana na historia yetu. Kazi kubwa na ya msingi inayofanyika katika kujifunza historia hiyo, ni kurithisha dhamira ya kujituma na kudumisha uhuru wa nchi yetu. Hivyo, ili kuendelea kukijenga Chama, na kuimarisha uwezo wa kuendelea kukamata dola barabara kwa namna endelevu, hapana budi ihakikishwe kuwa historia ya CCM inabeba pia jukumu la msingi la kusaidia:-

 

Kujua Chama kilikotoka, mahali kilipo na kinakoelekea katika misingi ya sera, itikadi, malengo na wanachama.

 

Kuunganisha wanachama na kuwaweka pamoja kiimani, kiitikadi na kiutendaji.

 

Wanachama kujitambua, kutambua wajibu na majukumu yao na kujenga moyo wa kujiamini na kujithamini.

 

Kuinua kiwango cha ushiriki wa wanachama wa CCM na wananchi katika kubuni na kutekeleza mkakati na mbinu sahihi za kutetea na kuendeleza Chama na taifa kufuatana na hali ya wakati na mahali.

 

Kuweka misingi ya kufanya tathmini na hivyo kuwa na uhakika katika kufanya maamuzi.

 

Kupanda mbegu bora za upendo, uzalendo na uchungu wa kweli kwa uhai wa CCM na taifa kwa ujumla.

 

Kuwa na majibu sahihi wakati wote kwa hoja mbalimbali zinazotolewa kuhusu Chama Cha Mapinduzi na taifa kwa ujumla.

 

Kuweka msingi wa kurithisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine maadili ya msingi wa uhai wa CCM.

 

Kuhifadhi kuweka na kueneza kumbukumbu sahihi ya historia ya Chama, nchi, mchango wa Waasisi na wanachama na kuhakikisha wapotoshaji hawapati fursa ya kueneza uongo.

 

1.3 CHIMBUKO LA HISTORIA YA CCM

 

Pamoja na kwamba Chama Cha Mapinduzi kuwa kilizaliwa rasmi tarehe 5 Februari, 1977, chimbuko lake linaanzia miaka mingi kabla, sambamba na historia ya uhai wa taifa la Tanzania. Mizizi ya historia ya CCM imo ndani ya harakati za kukataa ukoloni na usultani, zilizofanywa na wananchi wa Tanzania. Wahenga wetu kwa pamoja tangu enzi, walionyesha wazi kukataa kwao kutawaliwa. Historia ya Tanzania inao utajiri wa mifano mingi ya harakati hizo japokuwa zilijengwa katika misingi ya ukoo na ujirani, katika wilaya na mikoa mbalimbali hata kabla ya kuundwa kwa vyama vya TANU na ASP.

 

Wananchi hao waliotutangulia walikataa kunyonywa, kupuuzwa, kubaguliwa, kutawaliwa, kunyanyaswa na kugawanywa katika misingi ya rangi, kabila, dini, jinsia, nk. Utu na uhuru wao ulikuwa na thamani kubwa sana. Hivyo waliamua kupambana dhidi ya udhalimu huo. Baadhi ya mifano ya jitihada za mapambano ya awali ni Vita ya Majimaji huko Umatumbi na maeneo ya kusini, Mbiru huko Upare, Waluguru, Wameru, Wahehe na mengineyo huko Unguja, Pemba, Kanda ya Ziwa na katika jamii za wafugaji. Ari, utashi, uzalendo na dhamira ya kweli ya kutaka kujitawala vilivyojidhihirisha katika harakati hizo, viliotesha mizizi iliyoshikilia uhai wa vyama vya TANU na ASP.

 

2.0 TANU NA HARAKATI ZA KUPIGANIA UHURU WA TANGANYIKA

 

2.1 TANU ilizaliwa katika mazingira yaliyoandaliwa na Tanganyika African Association (TAA):

 

TAA iliundwa 1948 kufuatia tukio la kutengana kwa African Association (AA) ya Tanganyika na Zanzibar. AA ilizaliwa Dar es Salaam 1927 chini ya uongozi wa Cecil Matola akiwa Rais na Kleist P. Sykes akiwa Katibu. Malengo ya AA yalikuwa ni kupigania haki, maslahi na umoja wa Waafrika. AA ilikuwa na matawi yake makuu Dodoma na Zanzibar. Aidha, AA ilifungua matawi katika miji iliyokuwa makao makuu ya wilaya.

 

Katiba ya TAA ilitamka wazi kwamba Chama hicho hakikuwa na malengo ya kisiasa. Mwaka 1953 yalifanyika mabadiliko ya uongozi katika TAA. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alichaguliwa kuwa Rais wa TAA. Chini ya uongozi mpya, Katiba ya TAA ilionekana kwamba isingeweza kukidhi malengo ya kisiasa. Mwalimu alipewa jukumu la kuandaa Katiba mpya ya TAA ambayo ingezingatia malengo ya kisiasa. Baada ya uandaaji wa Katiba hiyo kukamilika, haja ya kubadili jina ilionekana dhahiri na majina mengi yalipendekezwa likiwemo la TANU. Nafasi ya TAA ilichukuliwa na TANU iliyozaliwa tarehe 7 Julai, 1954. TANU ilirithi matawi ya TAA, wanachama na viongozi wa TAA katika maeneo mengi.

 

Waasisi wa TANU ambao walihudhuria na kushiriki katika Mkutano wa kuzaliwa kwa TANU walikuwa 17:

 

Mwalimu J.K. Nyerere – Rais wa TAA/TANU

 

Geremano Pacha – Jimbo la Magharibi

 

Joseph Kimalando – Jimbo la Kaskazini

 

Japhet Kirilo – Jimbo la Kaskazini

 

C.O. Milinga – Jimbo la Mashariki

 

Abubakari llanga – Jimbo la Ziwa

 

L.B. Makaranga – Jimbo la Ziwa

 

Saadani A. Kandoro – Jimbo la Ziwa

 

Suleman M. Kitwara – Jimbo la Ziwa

 

Kisung’uta Gabara – Jimbo la Ziwa

 

Tewa Said Tewa – Jimbo la Mashariki

 

Dossa A. Aziz – Jimbo la Mashariki

 

Abdu Sykes – Jimbo la Mashariki

 

Patrick Kunambi – Jimbo la Mashariki

 

Joseph K. Bantu – Jimbo la Mashariki

 

Ally Sykes – Jimbo la Mashariki

 

John Rupia – Jimbo la Mashariki

 

TANU ilizaliwa baada ya Vita ya Pili ya Dunia:

 

 

 

Katika vita ya Pili ya Dunia (1939 – 1945), Watanganyika walishiriki wakiwa askari upande wa Waingereza. Katika kushiriki huko, baadhi yao walipigana vita nchi za nje, kwa mfano, India, Burma, Madagascar n.k. Wakiwa huko vitani walipata fursa ya kubadilishana mawazo ya kisiasa na askari wenzao waliokutana nao katika uwanja wa vita.

 

Baadhi ya askari hao wa Tanganyika waliporejea kutoka vitani walikuja na fikra mpya za ukombozi wa Mwafrika. Fikra hizi mpya zilioana na zile za Kituo cha Wasomi wa Kiafrika waliokuwa London. Kituo hicho kilijishughulisha sana na suala la ukombozi wa Mwafrika kupitia midahalo.

 

TANU ilizaliwa katika mazingira ya vyama vya ushirika:

 

Katika miaka 1950, wakulima walikwishajiunga na kuanzisha vyama vya kuuza mazao yao ya biashara ili waweze kupata bei nzuri kwa kupunguza gharama ya mtu wa kati ambaye alikuwa ni mfanyabiashara wa Kiasia. Baadhi ya Vyama vya Ushirika vilivyokuwepo kabla ya TANU ni:-

 

Kilimanjaro Co-operative Union Ltd (1933)

 

Ngoni – Matengo Co-operative Union Ltd. (1936)

 

Rungwe African Co-operative Union Ltd. (1949)

 

Bukoba Co-operative Union Ltd. (1950)

 

Lake Province Native Growers Association.

 

Kwa kuwepo vyama vya ushirika, ujumbe wa TANU kuwafikia wananchi ulirahisishwa. Wanachama wa vyama vya ushirika walijiunga na TANU. Wanachama na viongozi wa vyama vya ushirika waliunga mkono TANU katika madai yake ya kudai uhuru. Baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika walichaguliwa kuwa viongozi wa TANU katika ngazi ya Taifa. Kwa mfano:-

 

Ndugu Nsilo Swai

 

Sir George Kahama

 

Ndugu Jeremiah Kasambala

 

Balozi Paul Bomani

 

Ndugu John Mhavile.

 

TANU nayo iliunga mkono vyama vya ushirika katika madai yake ya bei nzuri ya mazao yao na kuondoa ushuru wa kahawa uliokuwa unatozwa na Serikali Kuu. Aidha, TANU ilihimiza na kuwahamasisha wananchi kuanzisha na kuimarisha vyama vya ushirika. Kazi hii ya kuhimiza na kuhamasisha wananchi kujiunga na ushirika iliendelea kufanywa na TANU hata baada ya Tanganyika kupata uhuru wake.

 

Baada ya Uhuru, TANU iliuona ushirika kuwa ni chombo cha kuleta maendeleo hivyo wananchi walihimizwa kuanzisha ushirika katika maeneo ambayo hayakuwa na vyama vya ushirika. Hali hii inaendelea hadi hivi sasa ambapo katika mfumo wa uchumi wa Soko, CCM inauona ushirika kuwa ni chombo cha kumwezesha mwananchi kiuchumi katika kumiliki na kuendesha uchumi wa Taifa lake

 

TANU ilizaliwa katika mazingira ya vyama vya wafanyakazi:

 

Lengo kuu la Vyama vya Wafanyakazi lilikuwa ni kutetea maslahi ya wafanyakazi. Baadhi ya vyama vya wafanyakazi ni:-

 

Chama cha Wafanyakazi Serikalini (1929)

 

Chama cha Makuli (1937)

 

Chama cha Wapishi na Madobi (1939)

 

Chama cha Wapishi na Watumishi wa Ndani

 

Chama cha Madereva

 

Chama cha Walimu

 

Chama cha Wafanyakazi wa Reli

 

Chama cha Wafanyakazi Mashambani

 

Chama cha Wafanyakazi Viwandani.

 

Vyama vya Wafanyakazi viliunda Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tanganyika Federation of Labour –TFL) tarehe 10 Oktoba, 1955.

 

Wafanyakazi kupitia vyama vyao walikuwa na madai yafuatayo:-

 

nyongeza ya mshahara

 

mapumziko ya mchana siku ya kazi

 

umri wa kustaafu na

 

kuondoa ubaguzi katika ajira na huduma za jamii.

 

Vyama vya wafayakazi vilisaidia kuvunja ukabila na hivyo kuwa chanzo cha umoja. Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi lilisaidia kueneza TANU kwa njia zifuatazo:-

 

Kila Chama cha Wafanyakazi chini ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TFL) kilitakiwa kuwashawishi na kuwahimiza wanachama wake kujiunga na TANU.

 

Kila mwanachama wa TANU aliyekuwa mwanachama wa Chama cha Wafanyakazi alitakiwa kulipa mchango wake wa kila mwezi kwa TANU.

 

Vyama vya Wafanyakazi, wakati mwingine kupitia TFL, viliweza kusaidia TANU kifedha fedha hizo zilitokana na michango ya hiari.

 

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi lilisaidia sana kuleta mwamko wa kisiasa miongoni mwa wafanyakazi.

 

Vyama vya Wafanyakazi vilifanya yote hayo kwa kuelewa kwamba uhuru ndio ungekuwa suluhisho la kweli la matatizo yao.

 

Kama ilivyokuwa kwa vyama vya ushirika, baadhi ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi walichaguliwa kuwa viongozi wa TANU. Mwaka 1958, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, Mzee Rashid Mfaume Kawawa, alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU. Toka wakati huo hadi hivi sasa, Mzee Kawawa amekuwa na uongozi uliotukuka katika TANU/CCM.

 

Kwa upande wake, TANU iliunga mkono madai ya vyama vya wafanyakazi na migomo ya wafanyakazi. Katika historia ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, mgomo wa wafanyakazi wa Shamba la Mazinde huko Tanga na mgomo wa wafanyakazi wa Kiwanda cha Bia Dar es Salaam ni miongoni mwa migomo maarufu.

 

Shamba la Mazinde lilikuwa mali ya bepari mmoja wa Kiingereza, mwanachama mashuhuri wa United Tanganyika Party (UTP) aliyewahi kushiriki katika kugombea na kushindwa na mgombea wa TANU katika Uchaguzi Mkuu wa Baraza la Kutunga Sheria mwaka 1958. Wafanyakazi katika Shamba la Mazinde walijiunga na Chama cha Wafanyakazi Mashambani (Tanganyika Plantation Workers’ Union – TPWU) ambacho kilikuwa kimeshirikishwa katika Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi. Mmiliki wa Shamba la Mazinde alikuwa na tabia ya kuwafukuza wafanyakazi walioonyesha kupinga UTP na walioamua kujiunga na Chama cha Wafanyakazi Mashambani. Katika harakati za kuwaunga mkono wenzao waliofukuzwa, wafanyakazi wote elfu tatu (3,000) waliamua kugoma na matokeo yake wote walifukuzwa kazi.

 

Jitihada za TFL kusuluhisha mgogoro huo kati ya Mwajiri na wafanyakazi zilishindikana. TFL na TANU kwa pamoja viliunga mkono mgomo wa wafanyakazi wa Shamba la Mazinde. TANU kupitia Mwalimu Nyerere ilitoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga kuwahifadhi wafanyakazi waliofukuzwa kazi. Wananchi waliitikia wito wa TANU na kuwapokea na kuishi nao. Aidha, TFL na TANU vilitoa wito kwa wananchi kususia shamba la Mazinde. Wafanyakazi hao hawakurejea kazini hata baada ya mmiliki kuwataka kufanya hivyo. Matokeo yake ni kwamba mmiliki huyu wa Shamba la Mazinde hakuchukua muda akafilisika na akarejea kwao Uingereza.

 

Huu ulikuwa ni ushindi wa TANU na TFL. TANU ilitambuliwa na wafanyakazi mashambani na iliendelea kuimarika. Kwa kuwa ngome ya UTP, na baadaye African National Congress (ANC) ilikuwa huko Tanga pigo hili lilisababisha kifo cha UTP na kuzorota kwa ANC.

 

Kuhusu mgomo wa Kiwanda cha Bia Dar es Salaam, mgomo ulianza Aprili hadi Juni, 1958. Mgomo uliwashirikisha wafanyakazi wapatao mia tatu (300). Wafanyakazi walikuwa wanadai nyongeza ya mshahara. Wafanyakazi wote waliogoma walifukuzwa kazi na mwajiri.

 

Katika kuonyesha mshikamano na wafanyakazi katika mgomo huu wa Kiwanda cha Bia, TANU ilichukua hatua zifuatazo:-

 

Ilitoa wito kwa nchi nzima kususia pombe zote za kigeni;

 

Iliwaomba wananchi wa Dar es Salaam kuwasaidia wagomaji kwa kuwachangia chakula na fedha;

 

Iliwaomba wananchi wenye nyumba Ilala kuwapokea wagomaji katika nyumba zao pasipo kuwatoza kodi ya nyumba.

 

Kama kawaida yao, wananchi waliitika wito na maombi ya TANU. Kwa kupitia migomo TANU ilizidi kuimarika miongoni mwa wafanyakazi.

 

2.5 TANU ilizaliwa katika mazingira ya kero na adha za wananchi kutoka Serikali ya Kikoloni:

 

 

Malalamiko hayo ya wananchi yalijidhihirisha katika maeneo yafuatayo:-

 

Upinzani huko Upare dhidi ya ulipaji kodi kulingana na mapato (Mbiru);

 

Wahehe kukataa kuogesha ng’ombe wao;

 

Waluguru kupinga juhudi za kuhifadhi mapori na kulima matuta;

 

Wafugaji (Wasukuma) kupinga kodi ya ng’ombe na kupunguza idadi ya ng’ombe, kumi kwa kila mia;

 

Wameru wapatao 3,000 walipinga kunyang’anywa ardhi yao na Serikali ya Kikoloni na kuwapa walowezi.

 

TANU ilitumia kero hizo za wananchi katika kuwaunganisha wananchi na kuwaelekeza namna ya kutafuta haki zao.

 

Kuhusu ardhi ya Wameru, Katika mkutano wake wa kwanza, TANU ilitoa tamko lifuatalo:-

 

“Mkutano huu unasikitika sana juu ya mambo yaliyofanywa na Serikali ya nchi hii huko Meru. Mkutano unakubali kwamba Serikali inayo mamlaka kuchukua ardhi ya raia hata kwa lazima ili ardhi hiyo iwe faida ya watu wote kama vile kupitisha reli, barabara, kujenga hospitali, shule au kutumia kwa jambo lingine la manufaa kwa wote. Lakini Serikali haina mamlaka kuchukua ardhi ya raia ili ardhi ile wapewe raia wengine waitumie kwa faida yao wenyewe … Mkutano huu unataka Serikali iwarudishie Wameru ardhi yao ama kuwalipa fidia kwa hasara walizopata kubwa, kwa kufukuzwa kama mahabusu, kama Baraza la Umoja wa Mataifa lilivyokubaliana.” (Historia ya Chama cha TANU 1954 hadi 1977, uk 36).

 

2.6 Kuenea kwa TANU na Kupata Ushindi:

 

Dhumuni la kwanza la TANU mwaka 1954 lilikuwa ni kuwatayarisha Watanganyika kujitawala na kujitahidi kwa bidii mpaka Tanganyika imepata uhuru na inajitawala. TANU ilibaini kwamba lengo lake kuu ni kupigania uhuru wa Tanganyika na silaha yake kubwa ni umoja hasa umoja wa Waafrika. Kwa mnasaba huo, TANU iliacha mlango wake wazi kwa Waafrika bila ya kujali kabila, dini, rangi, jinsia na majimbo yao. Toka mwanzo, msingi huu uliifanya TANU kuwa chama cha umma. Hata hivyo uamuzi wa kukifanya Chama cha TANU kuwa wazi kwa Waafrika tu ulikuwa ni uamuzi wa kimkakati tu. Haikukusudiwa kukifanya Chama hicho kuwa cha kibaguzi na kwa hakika kiliendelea kushirikiana na kuwaenzi Waasia na Wazungu walioafiki imani na madhumuni ya TANU.Miongoni mwa Waasia na Wazungu waliokuwa na mtazamo wa kizalendo katika shughuli za kisiasa ni Amir Jamal, Al-Noor Kassim, Derek Bryceson, Babra Johnson na Leader Stirling. Baada ya uhuru (1962), Waasia na Wazungu waliruhusiwa kuwa wanachama wa TANU.

 

Katika harakati za kuitangaza TANU, njia mbali mbali zilitumika:-

 

TANU ilifungua matawi katika maeneo mbali mbali ya nchi yetu.

 

TANU ilitumia mikutano ya hadhara katika kufikisha ujumbe wake kwa wananchi.

 

TANU ilitumia mikutano ya ndani ya wanachama.

 

TANU ilitumia vyombo vya habari, hususan magazeti, kama vile Sauti ya TANU, Habari za TANU na Mwafrika.

 

2.7 Jumuiya za TANU za Umoja wa Wanawake, Umoja wa Vijana na Wazazi zilifanya kazi kubwa katika kukieneza na kukiimarisha Chama.

 

TANU ilianzisha rasmi mwaka 1955 sehemu ya Wanawake wa TANU. Chama kilitambua kwamba mapambano ya kudai uhuru yasingeweza kufanikiwa bila ya kulitumia jeshi kubwa la Wanawake. Chama kilimpata Bibi Titi Mohamed na kumpa jukumu la kuwakusanya wanawake ili washiriki katika mapambano ya kudai uhuru. Sehemu ya Wanawake ilipewa majukumu yafuatayo:-

 

Kupata wanachama wa TANU wengi;

 

Kueneza Chama hasa vijijini kwa moyo wa kujitolea;

 

Kuona kwamba viongozi wa Chama wako salama/ulinzi wa viongozi na

 

Kukipatia Chama fedha kutokana na shughuli halali mbali mbali.

 

Katiba ya TANU ya mwaka 1954, sehemu ya sita, ilitoa nafasi kwa vijana kuunda umoja wao ili waweze kushiriki kwa ukamilifu katika mapambano ya kudai uhuru. Umoja wa Vijana ulikuwa na majukumu yafuatayo:

 

Kuwaandaa vijana katika uongozi;

 

Kuwahimiza vijana kujitolea kufanya kazi za TANU;

 

Kutekeleza shabaha za TANU;

 

Kuunda makundi ya starehe na maendeleo miongoni mwa wanachama kama vile, elimu, biashara na michezo;

 

Kukusanya habari na kufuatilia mwenendo wa kisiasa nchini;

 

Kushirikiana na vyama vingine vya vijana visivyo na upinzani kwa TANU.

 

2.8 TANU ilivyopambana na kuvishinda vikwazo na hila za Mkoloni

 

Jumuiya ya Wazazi (Tanganyika Parent’s Association – TAPA) iliundwa mwaka 1955 chini ya Ndugu Lawi Sijaona. TAPA ilikuwa ndiye mtekelezaji mkuu wa Azimio la Mkutano Mkuu wa Tabora lililohusu upanuzi wa elimu. Katika kutekeleza jukumu lake, TAPA ilifungua shule za msingi na sekondari nyingi nchini na kuendesha kisomo cha Watu Wazima. Huu ulikuwa mkakati wa makusudi wa kuwaandaa wananchi kushika madaraka baada ya uhuru.

 

Jinsi TANU ilivyozidi kuimarika ndivyo hivyo ilivyopambana na vikwazo na hila za Mkoloni:

 

Serikali ya Kikoloni ilipitisha Sheria mwaka 1953 ya kuwakataza watumishi wa Serikali wa mataifa yote kujiunga na vyama vya siasa. Aidha, Tangazo la Serikali Namba 2 la 1954 lilifafanua kuwa hata Sukuma Union kilikuwa ni Chama cha Siasa. Kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 6 la 1954, maafisa wote wa Serikali waliokuwa wanachama wa TANU na waliotaka kuendelea na utumishi serikalini walitakiwa kujiuzulu mara moja. Aidha, Sheria ya vyama vya siasa, 1954, ilitaka kila tawi la TANU lisajiliwe kabla ya kuandikishwa kisheria. Sheria hii iliiwezesha serikali ya mkoloni kusajili au kutokusajili tawi lo lote la TANU.

 

Mara tu baada ya TANU kuundwa, Rais wake Mwalimu Nyerere alitakiwa na Serikali ya Kikoloni achague moja kati ya mambo mawili ama kuendelea kuiongoza TANU au kujiuzulu uongozi wa TANU na kuendelea na kazi yake ya ualimu katika Shule ya Sekondari Pugu. Mwalimu aliamua kuendelea kuihudumia TANU hivyo akalazimika kujiuzulu kazi ya ualimu. Bila shaka, Serikali ya Kikoloni ilidhani kwamba Mwalimu asingejiuzulu ualimu. Katika suala hili, uamuzi wa Mwalimu haukuwa rahisi hasa kwa kuzingatia kwamba kazi ya ualimu ndio alikuwa ameisomea, riziki yake na ya familia ilitokana na ualimu na kwamba kuitumikia TANU wakati huo ilikuwa ni kupambana na Serikali ya Kikoloni na hii ilikuwa ni hatari kubwa. Kwa kujiuzulu ualimu, Mwalimu alipata nafasi kubwa zaidi ya kuihudumia TANU.

 

Mwalimu Nyerere mwaka 1958 alishitakiwa na Serikali ya Kikoloni kwa kosa la kuwakashifu District Commissioners wa Songea, Geita na Musoma. Kwamba kashfa hiyo aliifanya kwa kupitia makala aliyoiandika kupitia Gazeti la “Sauti ya TANU” Toleo Namba 29 la tarehe 27 Mei, 1958. Katika kesi hii iliyosikilizwa na Mahakama ya Dar es Salaam, Mwalimu alihukumiwa faini ya shs. 3,000/= (shilingi elfu tatu) au kifungo cha miezi 6. Mwalimu alilipiwa faini hiyo na TANU.

 

Serikali ya kikoloni pia ilijitahidi kadri ilivyoweza kuwatumia baadhi ya machifu kuwa chombo cha kuzuia uenezaji wa TANU. Machifu walipewa madaraka makubwa zaidi na zaidi ili wajisikie kuwa ni sehemu ya utawala na kwamba TANU ilikuwa na lengo la kuwakosesha maslahi yao. Mwaka 1957, Serikali ya kikoloni iliunda Baraza la Machifu wa Tanganyika (Territorial Convention of Chiefs). Kwa kuwatumia machifu, Serikali ya kikoloni ilitegemea kuwagawa Watanganyika kwa misingi ya ukabila ili kuweza kuwatawala wananchi kwa urahisi zaidi. Aidha, Serikali ya kikoloni ilikuwa na lengo la kuwagonganisha machifu na viongozi wa TANU.

 

Serikali ya kikoloni ilihimiza kuundwa kwa United Tanganyika Party (UTP) ndani ya Baraza la Kutunga Sheria mwaka 1956. UTP ilikuwa ni chombo na Sauti ya Serikali ya kikoloni kwa sababu zifuatazo:-

 

Uongozi wa UTP uliundwa na Wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria,

 

“Tanganyika Unofficial Members Organization (TUMO)”

 

Wajumbe hao waliteuliwa na Gavana na hivyo hawangeweza kupingana na siasa ya Serikali ya Kikoloni.

 

Licha ya hila na vikwazo vya mkoloni, TANU ilijikuta ina mtihani mgumu wa kuamua kushiriki ama kutokushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza mwaka 1958. Akifungua kikao cha kwanza cha Baraza la Kutunga Sheria mwaka 1956, Gavana Edward Twining alitangaza kuwa Serikali ilikuwa na mpango wa kufanya Uchaguzi Mkuu wa kwanza mnamo 1958. Sharti moja kubwa la uchaguzi huo lilikuwa kwamba kila mpiga kura apige kura tatu: moja kwa Mzungu, moja kwa Mwasia na moja kwa Mwafrika.

 

Suala hili la kura ya Mseto lilijadiliwa kwa undani katika Mkutano Mkuu wa TANU uliofanyika Tabora mwaka 1958 na kuhudhuriwa na Wajumbe 300 kutoka sehemu zote za Tanzania Bara. Ili kupata nafasi nzuri ya kujadili agenda hii, Mwalimu Nyerere aliomba asiwe Mwenyekiti wa kikao hicho, nafasi yake ilichukuliwa na Mwalimu Kihere kutoka Tanga.

 

Mwalimu Nyerere aliweza kuushawishi Mkutano kukubali kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza mwaka 1958. Hoja za Mwalimu zilikuwa ni kwamba kama TANU isingeshiriki, ingekuwa imeshindwa kwani isingekuwa na wawakilishi katika Baraza la Kutunga Sheria. Kujitoa katika uchaguzi huo kungekuwa na maana ya kujitoa katika uwanja wa mapambano ambao sasa ungemilikiwa na UTP. Uamuzi wa TANU kushiriki katika uchaguzi huo ulikuwa ni wa busara kwani wagombea wote waliosimamishwa kwa tiketi ya TANU walishinda na hivyo TANU kunyakua viti vyote vya wajumbe wa kuchaguliwa wa Baraza la Kutunga Sheria.

 

Matokeo ya kukubali kura ya mseto, aliyekuwa Katibu Mwenezi wa TANU, Ndugu Zuberi Mtemvu aliamua kuachana na TANU na kuanzisha African National Congress (ANC) mwaka 1958. Hata hivyo toka kuanzishwa kwake hadi kifo chake, ANC haikupata hata kiti kimoja katika Baraza la Kutunga Sheria. Aidha, Ndugu Mtemvu alibwagwa kwa kishindo na Mwalimu Nyerere katika kugombea Urais wa Jamhuri ya Tanganyika mwaka 1962.

 

Uchaguzi Mkuu wa pili ulifanyika mwaka 1960. Katika uchaguzi huo, TANU ilijikuta imefanikiwa kupitisha wagombea wake 58 bila ya kupingwa. Kati ya wagombea hao 58 waliopita bila kupingwa, 8 walikuwa Wazungu, 11 Waasia na 39 Waafrika. Tarehe 30 Agosti, 1960 ulifanyika uchaguzi katika sehemu nyingine ambako kulikuwa na zaidi ya mgombea mmoja katika jimbo la uchaguzi. Wagombea viti wote jumla walikuwa 25 kati ya hao 11 walisimamishwa na TANU na walishinda isipokuwa mmoja tu wa kiti cha Mbulu, Chifu Amri Dodo aliyeshindwa na Herman E. Sarwatt ambaye alikuwa mgombea binafsi. Hata hivyo, Sarwatt alikuwa ni mwanachama wa TANU.

 

Pamoja na vikwazo hivi Msimamo sahihi usioyumba uongozi bora umoja mshikamano ari na dhamira ya wananchi ya kutaka kujitawala vilikuwa chachu iliyosababisha TANU kupata ushindi wa kishindo na kutokana na ushindi huo, Gavana Richard Turnbull alimwomba Rais wa TANU, Mwalimu Nyerere kuunda Baraza la Mawaziri ambalo lilikuwa na jukumu la kuongoza nchi kwa jumla na kumshauri Gavana. Serikali ya Madaraka iliundwa na kuapishwa tarehe 3 Septemba, 1960. Tanganyika ilipata Serikali ya Ndani tarehe 1 Mei, 1961 na uhuru kamili tarehe 9 Desemba, 1961 na Mwalimu Nyerere kuwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanganyika huru.

 

2.9 Siri ya ushindi wa TANU

 

Uhuru wa Tanganyika ulipatikana katika kipindi cha miaka saba tu ya kudai uhuru. Kipindi hiki ni kifupi. Siri ya TANU ya ushindi ilitokana pamoja na mambo yafuatayo:-

 

Tanganyika ilikuwa chini ya Udhamini wa Umoja wa Mataifa tofauti na nchi kama Kenya, Uganda, Zambia na Malawi zilizokuwa makoloni moja kwa moja chini ya Serikali ya Kiingereza iliyokuwa na sauti ya mwisho. Chini ya udhamini huo watawala wa Kiingereza, walipaswa kuitawala nchi hii kwa mujibu wa masharti ya Umoja wa Mataifa kuhusu makoloni ya udhamini.

 

Nafasi ya Jamhuri ya Kisovieti (Urusi) (ilikuwa miongoni mwa mataifa manne makubwa) katika Umoja wa Mataifa ilisaidia kutoa msukumo kwa Umoja huo katika kufanikisha juhudi za TANU za kudai uhuru wa Tanganyika. Aidha, Urusi ilikuwa ni Mjumbe wa Baraza la Udhamini. Msimamo wa Urusi kuhusu makoloni ulikuwa thabiti kwamba makoloni yana haki ya kujitawala. Uhuru wa India, Pakistani na Ghana ulisaidia kutoa msukumo kwa makoloni kujipatia uhuru.

 

Lugha ya Kiswahili ilisaidia sana katika kuharakisha maendeleo ya siasa. Kiswahili kilisaidia kuwaunganisha wananchi na hasa kilirahisisha kazi ya viongozi wa TANU. Viongozi hao hawakuhitaji wakalimani wakati wa kuwahutubia wananchi katika mikutano ya hadhara. Lugha ya Kiswahili ilisaidia na inaendelea kusaidia katika kuleta umoja na mshikamano wa kitaifa.

 

Katika Tanganyika hapakuwepo na mtengano wa kijamii wenye nguvu. Tanganyika ilikuwa na makabila yapatayo 120 lakini kihistoria hapakuwa na utawala wa kikabila wa kugandamiza kabila lingine.

 

Tanganyika ilikuwa na walowezi wachache ikilinganishwa na nchi kama Kenya. Katika makoloni mengi uhuru wa wananchi ulicheleweshwa kutokana na siasa za walowezi ambazo msingi wake ni uchumi hodhi.

 

Umoja wa Vijana na Umoja wa Wanawake chini ya TANU, walitoa msukumo mkubwa katika kudai uhuru. Vikundi hivyo vilijawa na ari na moyo wa kimapinduzi; vilifanya kazi ya kujitolea usiku na mchana.

 

Vyama vya Wafanyakazi na Vyama vya Ushirika viliweza kuwabana vilivyo Wakoloni kwa njia ya migomo na ususiaji wa bidhaa.

 

Uongozi bora wa TANU, hususan uongozi wa Mwalimu Nyerere. Uongozi bora wa TANU ndio uliokipa Chama msimamo thabiti na kuwafanya wananchi kuwa na imani kubwa na TANU.

 

Aidha TANU iliweza kushinda changamoto katika sura ya hila na vikwazo kadhaa na kupata mafanikio kama vile:-

 

3.0 ASP NA HARAKATI ZA MAPAMBANO DHIDI YA UKOLONI WA KIINGEREZA NA USULTANI WA KIARABU

 

 

 

Mazingira ambamo ASP ilizaliwa:

 

 

 

ASP ilizaliwa katika mazingira yaliyokwisha andaliwa kisiasa na African Association (AA) na Shirazi Association (SA); vyama ambavyo vilikuwa nusu vya siasa na nusu vya kupigania maslahi ya Watumishi wa Kiafrika kazini. Katika mazingira hayo, waafrika na Washirazi walielewa kwamba:-

 

 

 

Adui wa Waafrika ni ukoloni wa Kiingereza na umwinnyi wa Kiarabu ukiongozwa na Sultani.

 

Umoja miongoni mwa Waafrika ni muhimu ili kujipatia uhuru wa kisiasa.

 

Ukoloni wa Kiingereza ulikuwa na nia ya kutoa uhuru kwa Waarabu wa Oman ambao walichukuliwa kwamba ndio wenye nchi.

 

 

 

Aidha, ASP ilizaliwa katika mazingira yaliyokuwa yamejaa manung’uniko dhidi ya ukoloni wa Kiingereza na ubwanyenye/umwinyi wa Kiarabu.

 

Miongoni mwa manung’uniko hayo ni:-

 

 

 

Kutokuwepo na demokrasia ya kweli katika utawala wa kikoloni.

 

Kutokuwepo na wawakilishi wa Waafrika katika baraza la Kutunga Sheria kuanzia mwaka 1926 hadi 1946

 

Ubaguzi katika kazi na huduma za jamii, hususan elimu na afya.

 

Ardhi ilikuwa inamilikiwa na kusimamiwa na Waarabu. Waafrika walikuwa manokoa katika mashamba ya Waarabu.

 

Sheria ya Serikali ya Kikoloni ya mwaka 1953 iliwazuia wafanyakazi Serikalini wasishiriki katika shughuli za kisiasa.

 

 

 

ASP ilizaliwa baada ya Zanzibar Nationalist Party (ZNP) au HIZBU kuwa imeundwa mwaka 1955. HIZBU ndicho chama kilichotoa upinzani mkubwa kwa ASP.

 

 

 

ASP ilizaliwa baada ya Vita Kuu ya Pili. Uingereza ilitoka vitani ikiwa maskini ajabu ikilinganishwa na kipindi kabla ya vita na haikuwezekana tena kuendelea kushikilia makoloni yake. Marekani ilizuka katika vita ikiwa Taifa lenye nguvu zaidi kuliko mataifa yote ya Ulaya Magharibi.

 

 

 

ASP ilizaliwa baada ya vyama vya siasa vingine kuwa vimeibuka katika nchi nyingine za Afrika hasa TANU ambayo ilikuwa na mahusiano ya karibu na ASP. Hata kabla ya ASP, kulikuwa na uhusiano wa kihistoria uliojengeka tangu kuanzishwa kwa AA Tanzania Bara na Zanzibar na vile vile kuendeleza ushirikiano huo kupitia TAA na AA ya Zanzibar. Hata wakati wa kuunganisha AA na SA na kuunda ASP, Rais wa TANU Mwalimu Nyerere alihudhuria Mkutano huo.

 

 

 

 Kuzaliwa na Kuimarika kwa ASP:

 

 

 

Wazo la kuunganisha nguvu za Waafrika liliwasilishwa kwenye Mkutano wa Pamoja wa African Association (AA) na Shirazi Association (SA) uliofanyika tarehe 5 Februari, 1957. Mkutano huo ulikubaliana kuunganisha AA na SA na kuanzisha Afro-Shirazi Party (ASP). Sheikh Abeid Amani Karume alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa ASP na Sheikh Thabit Kombo alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu.

 

 

 

Waasisi wa ASP waliohudhuria Mkutano huo na kupitisha uamuzi wa kuunganiisha AA na SA ni:-

 

 

 

African Association  (AA): Shirazi Association (SA):

 

 

 

1. Sheikh Abeid Amani Karume  1. Sheikh Thabiti Kombo

 

2. Sheikh Mtoro Rehani  2. Sheikh Muhidini Ali Omar

 

3. Sheikh Ibrahim Saadallah  3. Sheikh Ali Ameir

 

4. Sheikh Mtumwa Borafia  4. Sheikh Ameir Tajo

 

5. Sheikh Bakari Jabu  5. Sheikh Ali Khamis

 

6. Sheikh Rajab Swedi  6. Sheikh Mdungi Ussi

 

7. Sheikh Saleh Juma  7. Sheikh Haji Khatibu

 

9. Sheikh Abdullah Kasism Hanga  8. Sheikh Othman Sharif

 

9. Sheikh Ali Juma Seif

 

10. Sheikh Mzee Salehe Mapete.

 

 

 

Chimbuko la kuunganisha AA na SA lilitokana na Tangazo la Serikali ya Kikoloni kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Kwanza wa kuwachagua Wajumbe 6 kati ya 12 wa kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria Zanzibar (Legislative Council – LEGCO). Uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Julai, 1957. wajumbe 6 wengine walitakiwa kuteuliwa na Sultani. Bila ya kuungana isingekuwa rahisi kwa AA na SA kupata viti katika Baraza la Kutunga Sheria hasa kwa kuzingatia kwamba Waarabu walikwishaunda Chama chao cha siasa Novemba, 1955. Licha ya ASP kutaka kushiriki na kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa Julai, 1957 lengo kuu la ASP lilikuwa ni kudai uhuru kamili wa Zanzibar kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza na utawala wa kidhalimu wa Kisultani.

 

 

 

Msimamo wa ASP ulikuwa kwamba Zanzibar ni nchi ya Kiafrika na hivyo uhuru wa Zanzibar usingeweza kukamilika kama Usultani wa Kiarabu usingeondoka. Msimamo huu ulikuwa tofauti kabisa na ule wa HIZBU ambao ulitaka uhuru wa Zanzaibar akabidhiwe Sultani.

 

 

 

Licha ya lengo kuu la kisiasa la kuleta uhuru, ASP pia ilikuwa na malengo ya kiuchumi na kijamii. Miongoni mwa malengo hayo ni:-

 

Kugawa upya ardhi ili imilikiwe na wengi badala ya wachache tu;

 

Kutoa elimu bure kwa wote;

 

Kueneza huduma za afya;

 

Kuwapatia wananchi makazi bora;

 

Kuondoa dhuluma mbali mbali na;

 

Kujenga ujamaa na ushirika.

 

 

 

Uchaguzi Mkuu wa Kwanza Julai, 1957:

 

 

 

Katika uchaguzi huo, ASP ilipata viti 5 kati ya 6. Kiti hicho kimoja cha Stone Town kilichukuliwa na mgombea wa Muslim Association ambacho kilikuwa Chama cha Wahindi wasiokuwa Hindu. Ingawa HIZBU ilisimamisha wagombea katika majimbo yote 6 ya uchaguzi, hawakupata kiti hata kimoja.

 

 

 

Baada ya uchaguzi huo, Zanzibar ilitawaliwa na vituko. Serikali ya kikoloni ilimteua Ali Muhsin Barwani kuwa Waziri. Huyu alikuwa Rais wa ZNP (HIZBU) aliyeangushwa na Abeid Amani Karume kwa kura 3,328 dhidi ya kura 918 katika Jimbo la Ng’ambo. ASP iliwasilisha malalamiko yake kwa Balozi Mkazi wa Kiingereza dhidi ya uteuzi huo lakini malalamiko hayo yalipuuzwa. Hii ikiwa ni kielelezo cha upendeleo aliokuwa nao Balozi Mkazi wa Kiingereza kwa Waarabu chini ya ZNP.

 

 

 

Mwaka 1959 Sultan Khalifa bin Haroub alipata nafasi ya kutembelea Uingereza, mwanae Seyyid Abdulla ndiye akawa Sultani wa muda na wakati huo akajiunga na ZNP. Mwanae Sultan kujiunga katika Chama cha siasa ilikuwa ni mbinu ya kuwakandamiza Waafrika.

 

 

 

Sultani na Balozi Mkazi wa Kiingereza walijitahidi kwa nguvu zao zote kuiangusha ASP. Balozi Mkazi wa Kiingereza aliwaita Washirazi na kuwashawishi kuanzisha Chama chao wakati Sultani naye aliwashawishi Washirazi wajitoe katika ASP. Baadhi yao walishawishika. Kwa mfano, Ameir Tajo alikwenda kinyume na matakwa na maadili ya ASP kwa kumweleza Balozi Mkazi wa Kiingereza kwamba Zanzibar ipatiwe uhuru wake baada ya miaka 10. Kamati Kuu ya ASP ilihitaji uhuru wa Zanzibar upatikane mwaka 1960. ASP ilimfukuza Ameir Tajo uanachama na uongozi. Aidha, Sheikh Mohammed Shamte na Sheikh Ali Sharif Mussa walijiondoa kutoka ASP baada ya Sheikh Ameir Tajo kufukuzwa.

 

 

 

Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP) ilizaliwa mwishoni mwa mwaka 1959. ZPPP ilianzishwa na wanachama wa ASP waliofukuzwa na kujiondoa kutoka ASP. Rais wa ZPPP alikuwa Sheikh Mohammed Shamte. Miongoni mwa viongozi mashuhuri wa ASP waliounda ZPPP ni pamoja na Sheikh Ameir Tajo aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya ASP na Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria akiwa Mwakilishi wa Unguja Kusini na Sheikh Ali Shariff Mussa ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria akiwakilisha Pemba Kaskazini. Ikumbukwe pia kwamba Sheikh Mohammed Shamte alikuwa akiwakilisha Pemba Kusini katika Baraza la Kutunga Sheria. Kwa hiyo kuondoka kwa hao Wajumbe 3 kulikuwa na maana ya ASP kubakia na Wajumbe 2 katika

 

 

 

Baraza la Kutunga Sheria. Wajumbe hao wawili ni Sheikh Abeid Amani Karume akiwakilisha Jimbo la Ng’ambo na mwakilishi wa Unguja Kaskazini, Sheikh Daud Mahmoud.

 

 

 

Kitendo cha kuzaliwa ZPPP kilifurahisha sana HIZBU na Balozi Mkazi wa Kiingereza. Katika furaha hiyo, Balozi alitoa nafasi kwa Rais wa ZPPP, Sheikh Mohammed Shamte kwenda kutembelea Uingereza na Marekani.

 

 

 

Ziara ya Ian Macleod, Waziri wa Makoloni:

 

 

 

Ian Macleod alitembelea Zanzibar Desemba 1959 na alifanya mazungumzo na viongozi wa ASP, ZNP na ZPPP. Katika mazungumzo hayo, Macleod alikubali mambo mawili:-

 

 

 

(a) Tume iteuliwe kuchunguza Katiba (maendeleo ya kikatiba)

 

(b) Uchaguzi Mkuu wa pili uliokuwa umepangwa kufanyika Julai, 1960 uahirishwe hadi hapo Tume itakapokuwa imetoa mapendekezo yake.

 

 

 

Tume ya Hilary Blood iliteuliwa na kupata nafasi ya kusikiliza maoni ya viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa Jumuiya. Kama kawaida ya Tume, mapendekezo yalitolewa.

 

 

 

Mapendekezo ya Tume ya Sir Hilary Blood:-

 

 

 

(1) Sultan asijihusishe na mambo yoyote ya siasa kwa maana ya kujiunga na chama cha siasa au kusaidia chama cho chote cha siasa.

 

(2) Kuhusu muundo mpya wa Baraza la Kutunga Sheria, ilipendekezwa kwamba liwe na wajumbe 21 wa kuchaguliwa na 8 wa kuteuliwa. Aidha, ilipendekezwa kwamba Baraza jipya liwe na Spika badala ya kuongozwa na Balozi Mkazi wa Kiingereza.

 

(3) Baada ya uchaguzi mkuu, Zanzibar iwe na mfumo wa Wizara chini ya Waziri Mkuu asiyekuwa na mamlaka ya mwisho. Balozi Mkazi wa Kiingereza ndiye angekuwa na mamlaka ya mwisho.

 

(4) Pawepo na upande wa Upinzani katika Baraza la Kutunga Sheria na Kiongozi wa Upinzani apangiwe mshahara kamili.

 

(5) Zanzibar kufanya mipango ya kujiunga katika mazungumzo ya shirikisho la Nchi za Afrika Mashariki.

 

 

 

Uchaguzi Mkuu wa Pili Januari, 1961:

 

ASP, ZNP na ZPPP walishiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Pili uliofanyika Januari, 1961. Tangazo la tarehe 16 Januari, 1961 lililotolewa na Balozi Mkazi wa Kiingereza lilieleza wazi kwamba chama cho chote kitakachopata viti zaidi katika uchaguzi mkuu wa pili ndicho kitakachounda Serikali. Katika uchaguzi huo, majimbo ya uchaguzi yalikuwa 22 yaani majimbo 13 Zanzibar na majimbo 9 Pemba.

 

Matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa ifuatavyo:-

 

ASP – viti 10 (viti 2 Pemba na 8 Unguja)

 

ZNP – viti 9 ( viti 4 Pemba na 5 Unguja)

 

ZPPP – viti 3 (viti 3 Pemba na 0 Unguja).

 

Kwa mujibu wa matokeo hayo, mshindi alikuwa ni ASP. Hata hivyo, matokeo hayo yalibadilika baada ya Wajumbe 2 wa ZPPP Sheikh Mohammed Shamte na Sheikh Bakari Mohammed Bakari kuamua kujiunga na ZNP na Mjumbe mmoja Sheikh Ali Shariff Mussa kujiunga na ASP.

 

Kwa kuzingatia kwamba ASP na ZNP walikuwa na viti sawa katika Baraza la Kutunga sheria, uamuzi ulifikiwa wa kuunda Serikali ya Mseto ambayo ilitakiwa kudumu kwa muda wa miezi sita.

 

Uchaguzi Mkuu wa Tatu Juni, 1961:

 

Katika uchaguzi huo, majimbo ya uchaguzi yaliongezwa toka 22 hadi 23. Jimbo jipya la uchaguzi lilikuwa Mtambile, Pemba Kusini ambapo ZPPP ilikuwa na nguvu. ASP, ZNP, ZPPP vilishiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Tatu. Hata hivyo,

 

ZNP na ZPPP walikuwa na makubaliano kwamba anaposimamishwa mgombea wa ZNP asisimamishwe mgombea wa ZPPP na kinyume chake. ASP ilisimamisha wagombea wake katika majimbo yote 23 ya uchaguzi.

 

Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Tatu uliofanyika tarehe 1 Juni, 1961:

 

ASP – viti 10 (Unguja 8 na Pemba 2)

 

ZNP – viti 10 (Unguja 5 na Pemba 5)

 

ZPPP – viti 3 ( Unguja 0 na Pemba 3)

 

Kuhusu kura, waliojiandikisha kupiga kura ni 94,218 na waliopiga kura ni 90,595 sawa na asilimia 96.15. ASP ilipata asilimia 49.9 ya kura zote zilizopigwa, ZNP asilimia 35.0, ZPPP asilimia 13.7 na kura zilizoharibika zilikuwa asilimia 1.4

 

Matokeo haya yanaonyesha kwamba ZNP na ZPPP kwa pamoja walipata viti 13 na ASP viti 10. Balozi Mkazi wa Kiingereza alimwomba Sheikh Ali Muhsin Barwani, Rais wa ZNP kuunda Serikali ya madaraka ambaye pia alitoa nafasi hiyo kwa Sheikh Mohammed Shamte, Rais wa ZPPP kuwa Waziri Mkuu.

 

Uchaguzi Mkuu wa Tatu ulitawaliwa na vurugu:-

 

Baadhi ya wapiga kura walipiga kura mara mbili.

 

Katika baadhi ya masanduku kura zilitumbukizwa kabla ya upigaji kura.

 

Siku ya uchaguzi tarehe 1 Juni, 1961 kulikuwa na fujo iliyosababisha mapigano kati ya wafuasi wa ASP na ZNP. Inakisiwa kwamba watu wapatao 400 walijeruhiwa na 68 walikufa. Machafuko hayo yalipamba moto zaidi tarehe 2 Juni , 1961 baada ya taarifa kuwafikia wanachama wa ASP kuwa Serikali ya Madaraka ilikuwa imeundwa na ZNP pamoja na ZPPP. Vikosi vya kuzuia fujo kutoka Kenya na Tanzania Bara ilibidi viende Zanzibar kuzuia fujo.

 

Mkutano wa kwanza wa Katiba ulifanyika London Machi, 1962. ASP iliongozwa na Mzee Karume na Othman Shariff wakati ZNP na ZPPP iliongozwa na Ali Muhsin Barwani (ZNP) na Mohammed Shamte (ZPPP). Baada ya Mkutano huo, Umma Party chini ya Abdurahaman Mohammed Babu ilizaliwa. Umma party ilikuwa na fikra za kimapinduzi, hususan fikra za kikomunisti. Babu alijitoa ZNP na hili lilikuwa ni pigo kwa chama hicho.

 

Uchaguzi Mkuu wa Nne Julai, 1963:

 

Majimbo ya uchaguzi yaliongezwa toka 23 hadi 31 yaani majimbo 17 Unguja na Majimbo 14 Pemba. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Zanzibar, watu wazima wote (miaka 18 na kuendelea) waliruhusiwa kupiga kura bila ya vikwazo vya kisomo na kipato. Uchaguzi ulifanyika chini ya ulinzi wa majeshi ya Kiingereza yaliyochukua sura ya mazoezi ya kivita kuliko uchaguzi.

 

Matokeo ya uchaguzi huo:-

 

ASP – viti 13 (Unguja 11 na Pemba 2)

 

ZNP – viti 12 (Unguja 6 na Pemba 6)

 

ZPPP – viti 6 (Unguja 0 na Pemba 6)

 

Kuhusu kura, ASP ilipata kura 87,085 sawa na asilimia 54.21; ZNP na ZPPP kwa pamoja zilipata kura 73,559 sawa na asilimia 45.79 ya kura zote halali zilizopigwa.

 

Kwa matokeo hayo, Sheikh Mohammed Shamte alitakiwa na Balozi Mkazi wa Kiingereza Kuunda Serikali ya Ndani tarehe 17 Julai, 1963. Mkutano wa Pili wa Katiba ulifanyika London kuanzia tarehe 20 hadi 24 Septemba, 1963 na Zanzibar ilipewa uhuru wake wa bandia tarehe 10 Desemba, 1963 kwa mujibu wa makubaliano ya Lancaster House – London.

SAMIA (1).jpg
bottom of page